MIL 58/- ZAPATIKANA MECHI YA SIMBA, MGAMBO
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na
Mgambo Shooting Stars iliyochezwa jana (Septemba 18 mwaka huu) katika Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam
imeingiza sh. 58,365,000.
Watazamaji 10,241 walikata tiketi kushuhudia mechi
hiyo namba 23 ya VPL msimu wa 2013/2014 iliyomalizika kwa wenyeji Simba kuibuka
na ushindi wa mabao 6-0.
Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh.
8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh.
13,839,327.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh.
8,903,135.59.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja
sh. 7,036,946.16, tiketi sh. 2,548,890, gharama za mechi sh. 4,222,167.70,
Kamati ya Ligi sh. 4,222,167.70, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
2,111,083.85 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,641,954.10.
MIKATABA YA MAKOCHA VPL, FDL YATAKIWA TFF
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa siku 14 kwa klabu za Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) na za Ligi ya Daraja la Kwanza (FDL) kuwasilisha mikataba ya
makocha wao.
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana Septemba 12 mwaka huu
imebaini klabu nyingi hazijawasilisha mikataba ya mabenchi yao ya ufundi, kitu ambacho ni matakwa ya
kikanuni. Siku hizo 14 zimetolewa kuanzia Septemba 17 mwaka huu.
Kwa
klabu ambazo zitashindwa kuwasilisha mikataba hiyo na vielelezo vingine ndani
ya mudau huo zitachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)