MAELFU YA WATU WA MUNGU WAANZA MAISHA MAPYA KATIKA IBADA YA JUMAPILI NA MCHUNGAJI JOSPHAT GWAJIMA
Ibada ya Jumapili
ya Tarehe 12.01.2014 katika Nyumba ya Ufufuo na Uzima Kawe yawa ya
Manufaa makubwa sana kwa Maelfu ya watu waliofika Ibadani, ni Baada ya
Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima kutangaza rasmi kuwa ni siku ya,
kufanya maombi na watu kujiweka huru dhidi ya matatizo na laana za
familia.
SOMO: MATATIZO YA FAMILIA/UKOO
Na. Mch Josephat Gwajima
1 Mambo ya Nyakati 1:1-54
Ni kitabu cha kushangaza sana kwenye
biblia sababu kinaelezea tu Fulani akamzaa Fulani, ni kitabu kilichokuwa
inanipa taabu sana kukisoma kwenye biblia sababu majina mengine ni magumu hata
kuyatamka, nikawa najiuliza hiki kitabu kinamaanisha nini na kwanini
kimeandikwa kwenye biblia, nilikuwa sielewi ni nini mtu unaweza kujifunza kwa
kuambiwa huyu akamzaa huyu.
Niliposoma kwenye 2 Timotheo 3:16
nikaona kila andiko lililoandikwa lafaa kwa mafundisho, nikajiuliza sasa haya
majina ya watu kwenye hiki kitabu yanatufundisha nini? Nilipokuwa natafakari
kitabu cha mambo ya nyakati nikapata shock (mshtuko) baada ya kusoma Mathayo 1:1-17 nikaona kitabu hiki
kimeanza kwa kuandikwa hiki ni kitabu cha ukoo wa Bwana yesu, nikajiuliza hee
hivi Yesu tena ana ukoo.
Nilipoanza kufuatilia huyu Mungu
anataja ukoo tena kwanini, 2 Wakorintho
5:17 hata imekuwa mtu akiwa ndani ya kristo amekuwa kiumbe kipya, sasa haya
mambo ya ukoo nini tena, niliposhuka kidogo nikaona haya ndiyo makabila 12 ya
Yakobo, nikashangaa zaidi kumbe Mungu anajishughulisha na makabila tena. Hapo
ndipo nikaanza kujifunza maisha ya mtu anayoishi leo, kama hauishi maisha
yanayo mpendeza Mungu maisha yako yatakuwa sawasawa na kabila au ukoo anaotoka.
Nikagundua kumbe kuelezea mambo ya familia hakuna tatizo maana hata Mungu yeye
mwenyewe ameelezea sana kwenye biblia.
Nikaanza kufuatilia baadhi ya familia
nikaona hata usome vipi huwezi kupata upenyo wa maisha, hata Mungu akikuinua kukupeleka
ulaya litatokea jambo Fulani litasababisha urudi tu sababu familia hii
hawaruhusiwi kupenya, familia hawaruhusiwi kutajirika, familia hawaruhusiwi
kumuriki nyumba, familia hawatakiwi kumiriki magari.
Unaweza kuwa umeokoka, lakini kama
hujadili na haya mambo ya familia utaingia mbinguni ukiwa umechoka,
umekung’utwa kwelikweli, umeokoka lakini unaishi maisha magumu kweli, unajiuliza mbona kwenye Mathayo 11:28 imeandikwa njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na
wenye kulemewa na mizigo nami nitakupumzisha, unashangaa mbona mimi sipumziki,
kumbe unatoka ukoo wa taabu wenye kulemewa na mizigo na laana (huo ni ukoo wa
kutokupumzika).
Hebu jaribu kuangalia maisha ya baba
yako na namna alivyo/anavyo malizia maisha yake, kama hakuna jitihada za ziada
na wewe utamalizia maisha vile vile. Yesu alikuja ili tukatae kuwa na maisha
kama waliyonayo baba/babu zetu, wewe umemuamini Yesu ili akuondolee yale maisha
aliyoishi baba yako. Usiseme ukoo wetu sio ukoo wa viongozi, ukoo wetu
hatufanikiwagi, ukoo wetu wanakufaga na umri mdogo, usiseme maneno hayo. Useme
mama yangu alimaliza hivi lakini mimi nasimama na Bwana Yesu naamua kwenda
beyond average, naamua kwenda mbele Zaidi. Usifuate kawaida wewe ukishakuwa
umeokoka hauendi kwa kawaida za binadamu.
Ndio maana tunavoanza kuomba tunasema
Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo hapa tunakuwa tunajiungamanisha na utajiri na
Baraka zote za Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Kabla ya Ibrahimu kulikuwepo na kina
Serugi, Tera na kina Nahori lakini hatuanzii huko maana Serugi alikuwa na
matatizo yake, Ibrahimu alitengwa na jamaa zake akaambiwa aende kwenye nchi
atakayokabidhiwa. Wokovu ni kutengwa, kutengwa na taratibu za ndugu, jamaa,
umasikini na mabalaa ya familia. Hivyo ukishaokoka tu maana umetengwa, hupaswi
kuwa kama alivyokuwa mama yako au baba yako au babu yako uende extra mile na
pale walipoishia walipokutangulia.
Sababu
itakayokufanya ukimbie kwa nguvu zote kwenda mahala pengine
Mwanzo 9:18-26
“…Hamu ndiye baba wa kanaani…”,
“…Hamu baba wa kanaani akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili
waliokuwa nje…”
Ukisoma hayo maandiko utaona Hamu
amefanya kosa na baba yake akamlaani kanaani na kizazi chake, na ukiendelea
kusoma biblia utaona hiyo laana inavyozidi fuatilia kizazi cha kanaani. Kumbe
hata leo kuna matatizo ambayo mtu unaweza kuwa nayo, sio kwamba yamesababishwa
na maisha yako unayoishi leo hapana, bali yamesababishwa na makosa waliyo fanya
babu wa ukoo, hiyo laana waliyolaaniwa ndiyo inayoendelea kukutafuna hii leo.
Nuhu akalevuka kutoka katika ulevi
wake akamlaani kanaani, kanaani analaaniwa kwa kosa la baba yake, aliyeona uchi
wa baba ni Hamu lakini laana ikamuangukia kanaani ambaye ni motto wa Hamu. Hapa
tunajifunza kile kilichofanyika na mababu kina sambaa kwenye ukoo na vizazi
vyote vijavyo, kama ni laana itasambaa kwenye kizazi chote, kama ni Baraka
itasambaa kwenye kwenye vizazi na vizazi.
Hebu
tuangalie maisha ya watoto waliozaliwa na kanaani
Mwanzo 10:15-19
Ukisoma hapo utaona kabila za
wakaanani zikatawanyika na hata sodoma na gomora ilitokea hapo kwenye ukoo wa
kanaani, unajiuliza hawa watu wa sodoma na gomora kwanini wanatenda uovu huu,
kumbe ni laana ambayo imeendelea kuwafuatilia, hata kuteketea.
Kutoka 3:17
Mungu anasema atawapandisha watu wake
kutoka katika mateso ya misri na kuwaingiza katika nchi ya mkaanani nchi
iliyojaa asali na maziwa. Utagundua hapo, hawa wakaanani wananyang’anywa nchi
yao na watu wa Mungu.
Kutoka 23:23 atawakatilia mbali wa
Yebusi, unajiuliza hawa watu wamekosa nini mpaka wapate mateso yote haya, tunagundua
ni lile kosa la Hamu kuona uchi wa baba yake, kosa hawakufanya hawa ukoo wa
Kanaani lakini ndio laana inaendelea kuwafuatilia.
Kutoka 33:2 “…Nitawafukuza…” Kumbe
kufukuzwa ni dalili ya laana
Kumb 20:17
Lakini uwaangamize kabisa Mhiti, na
Mwamori, na Mkaanani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi kama alivyokuamuru Bwana
Mungu wako. Utaona hapa laana inawafanya hawa watu waangamizwe kabisa, wengine
hata hawajui kulikuwa na Hamu ambaye alitenda kosa, lakini laana inaenda nao,
na kamwe haiwaachi. Nawe ndivyo ilivyo kuna laana inakufuatilia ambayo leo
lazima tuifanyie kazi.
1 Petro 1:18 “…Mwenendo wenu usiofaa
mliupokea kutoka kwa baba zenu…” Kumbe kuna mambo yasiyofaa yanayowapata watu
leo yalitoka kwa baba zao.
Mambo yaliyokupata kwenye maisha
yasikuzuie kupaa kwenda kwenye kesho yako, yote yaliyokupata yalikuwa ni
kukunoa uwe upanga mkali kwa ajili ya kesho yako.
Inawezekana leo una laana sababu ya
makosa waliyofanya babu zako, babu yako alitesa wenye haki, babu yako alifanya
mauaji akalaaniwa na laana inaendelea kwako hadi leo, leo ujitenge na laana za
familia, Ibrahimu alitengwa na jamaa na ndugu zake akatangaziwa Baraka na
kizazi chake chote hata kuzaliwa kwa Bwana Yesu.
Tanzania maeneo ambayo Mungu asiye
Yehova alipoabudiwa kwa muda mrefu ndio masikini kuliko maeneo yote, hiyo ni
kwa sababu ya laana ya kuabudu miungu mingine “Biblia inasema usimuabudu Mungu
mwingine ila mimi Zaburi 81:9” laana hiyo inakufanya uwe replaced Mungu
anakutoa na kumpa mwingine. Unapomuabudu Mungu mwingine ambaye sio Yesu unashangaa
watoto wako wanaanza kuondolewa, watoto wako wanaondolewa ni laana hiyo, wakati
mwingine unaamua wewe mwenyewe kuacha wenzako wanamiriki.
Namna nzuri ya kutoka kwenye ukoo ni
kutoka kama alivyofanya Ibrahimu akaambiwa toka leo kwa jamaa na ndugu zako
nenda mpaka nchi nitakayokuonyesha. Kutoka kwetu leo kwenye familia sio kukataa
familia, tunatoka kwa namna ya rohoni, tunajitenga na laana zote za familia,
unapofanya hivyo mashetani waliotawala familia yako kwa muda mrefu wanakosa
nguvu ya kukufuatilia.
Kila unapokataa kwenye ulimwengu wa
roho unavunja kitu, unabomoa kitu, na mashetani waliotumwa kulinda ukoo
wanakimbia wanajua huyu mtu katukataa.
Leo ukatae na kuhama kwenye ukoo wa
laana, ukoo wa umasikini, ukoo wa balaa, uhamie ukoo wa Ibrahimu, Isaka na
Yakobo, ukoo wa Bwana Yesu. Jitenge na mikosi yote, umasikini kwa jina la Yesu.
Ufanye hivyo kwa kumaanisha, na hakika yake utabadirika, hutakuwa kama ulivyo
kwa jina la Yesu.