http://www.mkcomputertweaks.com/mkgroup/fkbmksb.gifMatangazo

Tangaza nasi: mkatedaniel@gmail.com, +255 7666-00 69 70, +255 655-00 69 71, +255 787- 249594

Usilikose kila Jumapili

Jumatatu, 25 Machi 2013

Taifa Stars yatoa onyo Afrika, yainyuka Morocco 3-1

Mbwana Samata akishagilia moja ya mabao yake jana
MBWANA Samata alifunga mara mbili na Thomas Ulimwengu aliongeza jingine wakati timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, ilipotoa onyo kwa miamba ya soka Afrika baada ya kuisambaratisha Morocco kwa magoli 3-1 katika mechi ya Kundi C la kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Ulikuwa ni ushindi wa tatu mfululizo dhidi ya miamba ya soka katika bara hili baada ya kuwalaza kwa bao 1-0 waliokuwa mabingwa wa Afrika, Zambia katika mechi ya kujipima nguvu wakati wakienda kutetea taji lao nchini Afrika Kusini, kabla ya kuwabwaga Cameroon 1-0 katika mechi nyingine ya kirafiki.
Ushindi wa jana ulimaanisha kwamba Stars inaendelea kushikilia nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi C kwa kufikisha pointi sita, moja nyuma ya vinara Ivory Coast ambao nao juzi walishinda 3-0 dhidi ya Gambia mjini Abidjan. Magoli ya Ivory Coast yalifungwa na Yaya Toure, Wilfred Bonny na Salomon Kalou.    
Stars sasa imeshinda mechi mbili baada ya awali kuifunga Gambia 2-1 jijini Dar es Salaam kabla ya kulala 2-0 ugenini dhidi ya Ivory Coast. Mbali na kuzifunga Tanzania na Gambia, vinara wa Kundi C, Ivory Coast walishikiliwa kwa sare ya 2-2 ugenini Morocco.
Morocco wanaendelea kushika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 2 baada ya awali pia kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Gambia, ambao waganda mkiani wakiwa na pointi moja.
Matokeo ya jana yalikuwa ni kisasi kizuri cha Oktoba 9, 2011 ambapo Morocco waliifunga Tanzania idadi kama hiyo ya magoli 3-1 na kuifanya Stars ngazi ya kuelekea kwenye fainali ya AFCON 2012, ambapo magoli ya Morocco yakifungwa Adel Taarabt, Marouane Chamakh na Mbark Bousoufa huku goli la kufutia machozi la Stars likifungwa Abdi Kassim 'Babi'.
Kocha wa Stars, Kim Poulsen aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri akisema walicheza kwa tahadhari sana kwa kutambua kuwa Morocco inaundwa na wachezaji wengi wazoefu wanaocheza kwenye klabu za Ulaya.
"Tulicheza vizuri zaidi katika kipindi cha pili kwa sababu tulishajua udhaifu wao," alisema Poulsen, ambaye tayari amepewa ofa ya mkataba mpya ili ausaini baada ya wa sasa unaomalizika Mei.
Kocha wa Morocco, Rachid Rachid Taoussi alisema Tanzania walicheza vizuri zaidi yao kwa sababu walikuwa mbele ya mashabiki wengi na kwamba goli la mapema katika kipindi cha pili liliwagharimu na akaitaja kadi nyekundu aliyopewa nahodha wake Achchakir Abderrahim iliwamaliza kabisa.
Abderrahim alipewa kadi mbili za njano zilizofuatana baada ya kwenda kumbwatukia refa Helder Martins wa Angola kufuatia Morocco kufungwa goli la tatu katika dakika ya 80. Alionywa kwa njano ya kwanza, akaendelea kumbwatukia, akaongezwa njano nyingine.
Morocco walioonekana kucheza vyema katika kipindi cha kwanza ambacho walipata kona nne dhidi ya moja ya Stars, hata hivyo dakika 45 zilimazika matokeo yakiwa 0-0.
Wenyeji walianza kipindi cha pili vyema kwa kubadili mfumo kutoka 4-5-1 na kuwa 4-4-2 baada ya kumpumzisha kiungo Mwinyi Kazimoto na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji Thomas Ulimwengu ili mbele awe pacha wa 'mdunguaji' mwenzake wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Samata. 
Mabadiliko hayo ya kocha Poulsen yalizaa matunda ya haraka pale Ulimwengu alipofunga goli la kuongoza kwa kutumia mpira wake wa kwanza kuugusa uwanjani katika dakika ya 46 baada ya kutokea piga nikupige katika lango la Morocco.
Ushirikiano wa Samata na Ulimwengu uliendelea kuzaa matunda pale Samata alipoifungia Stars goli la pili katika dakika ya 66. Mpira ulianzia kwa Athuman Idd 'Chuji' aliyekuwa ameingia kuchukua nafasi ya Mrisho Ngassa. Chuji alipiga pasi ndefu kuelekea kwa Ulimwengu. Wakati mabeki wakikimbia haraka kumdhibiti Ulimwengu, mshambuliaji huyo aliuruka mpira na kuwapoteza mabeki na pasi hiyo kumfikia Samata aliyejikuta amebaki peke yake na kipa Lamyaghri Nadir, akamchagua kwa kupiga shuti lililopita kushoto kwa mlindamlango huyo wa Wydad Cassanlanca.
Samata alikamilisha ushindi mnono zaidi wa Stars katika miaka ya karibuni kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia krosi ya Ulimwengu iliyodhirihirisha makali ya ushirikiano wa wawili hao wa TP Mazembe katika dakika ya 80.
Wakiwa 10, Morocco walicharuka na kupata goli la kufutia machozi lililofungwa na Abdourazouk Hamza anayechezea klabu ya Raja Cassablanca akimalizia mpira wa kona katika dakika ya 90.
Baada ya mechi, kocha wa makipa wa Stars, Juma Pondamali aliyeonekana kujawa na furaha, aliwaongoza wachezaji kucheza "kiduku" na kisha akasema "Tanzania imewanyanyasa sana Morocco leo".
Vikosi vilikuwa; Stars: Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Salum Aboubakar "Sure Boy", Mrisho Ngassa/ Athumna Idd 'Chuji' (dk. 64), Frank Domayo, Mbwana Samata/ John Bocco 'Adebayor' (dk. 90), Mwinyi Kazimoto/ Thomas Ulimwengu (dk.46) na Amri Kiemba.
Morocco: Lamyaghri Nadir (Wydad Cassablanca), Bellak Hdar Younes (Far Rabat), Hafid Abdelilah (Raja Cassablanca)/ Ambrabat Noureddenne (Galatasaray, Uturuki) (dk.78), Bergdich Zakarya (Lens, Ufaransa), Achchakir Abderrahim (Far Rabat)/ Elarabi Yousser (Granada, Hispania) (dk. 56), Hammal Younes (Far Rabat), Barrada Abdulaziz (Getafe, Hispania), Eladoua Issam (Victoria, Ureno), Chafn Kamal (Brest, Ufaransa), Belghazouani Chahir (AC Ajaccio, Ufaransa) na Abdourazouk Hamza (Raja Cassablanca)