ILI
kuwapa hamasa Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi wa Tanzania (JWTZ) wanaoenda kulinda
amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya kondo (DRC), benki ya CRDB imetoa msaada wa
vifaa vya michezo kwa askari hao vikiwa na thamani ya Sh.milioni 6.8.
Msaada
huo ulitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Dk. Charles Kimei kwa niaba
ya benki yake, na kumkabidhi Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Samweli
Ndomba, aliyepokea kwa niaba ya mkuu wa majeshi nchini.
Akizungumza
katika makabidhiano hayo, Dk Kimei alisema vifaa hivyo vya michezo vinatolewa
kwa ajili ya wanajeshi wanaoenda kulinda amani DRC ili kuweza kuburudika katika
michezo wakati wa mapumziko.
“CRDB
inajua nyie ni wateja wetu wazuri, hivyo tumeamua kutoa msaada huu kwa
wanajeshi wanaoenda kujilinda amani ili kuweza kuwapa hamasa vijana wetu
watakapokuwepo huko,” alisema Dk. Kimei.
Vifaa
hivyo vilivyotolewa na benki hiyo ni jezi za soka, netiboli, khanga na vitenge kwa
ajili ya wanajeshi wa wanawake watakaokuwa wakicheza ngoma wakati wa mapumziko.
Akipokea
msaada huo, Luteni Jenerali Ndomba alianza kwa kuishukuru benki hiyo kwa kutoa
vifaa hivyo wakati wanajeshi wakijiandaa na safari ya kuelekea DRC.
“Si
mara yenu ya kwanza kutoa vifaa kama hivi, hata wakati ule vijana wetu walipokuwa
wakilinda amani Darfur, mlitupa msaada kama huu…tunashukuru sana kwa hilo, na
pia msaidie hata kutoa vifaa kwa timu za majeshi za hapa nyumbani ” alisema
Luteni Jenerali Ndomba.
Aidha,
Ndomba aliishukuru benki hiyo kwa kuweza kuahidi kutoa mikopo ya riba nafuu ya
nyumba kwa wanajeshi wa jeshi lake.