Serikali ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo imesema majeshi yake kwa kushirikiana na kile
kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa kilichopewa uwezo wa kupambana na
waasi wa M23 kimewapiga waasi hao katika ngome yao ya mwisho.
Msemaji wa Serikali, Lambert Mende ameiambia BBC
kuwa wapiganaji waliobaki wa M23 wanaweza wakawa wamekimbia, wamevuka
mpaka au wamejisalimisha.Mende amesema kikosi maalum cha majeshi ya nchi hiyo kimeharibu silaha za waasi hao usiku kucha na inasadikiwa kiongozi wa kijeshi wa kundi hilo la M23, Sultani Makenga ni miongoni mwa waliovuka mpaka na kuingia Rwanda au Uganda.
Wakati huo huo, viongozi wa nchi za SADC wanaokutana nchini Afrika Kusini wamezungumzia mgogoro wa Jumhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuwataka viongozi wa kundi la waasi wa M23 kutangaza kusimamisha mapigano.
Taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo imesema kama waasi hao watachukua hatua hiyo mkataba wa amani unaweza kusainiwa ndani ya siku tano zijazo.
CHANZO: BBC