KOCHA wa timu ya Rhino Rangers ya Tabora ambayo itashiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao, hajashangazwa na adhabu iliyotolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ya kumfungia mechi sita na kulipa faini, kwa madai ndio mfumo wa soka la Bongo.
Akizungumza na blog ya Kwetu Mbamba-bay, Renatus Shija alisema hajashangazwa na adhabu hiyo kwani ni mfumo wa soka la Tanzania ambao huendeshwa ‘kimajungu’, na mafanikio aliyoyapata aliamini lazima yataingi dosari.
“Wameamua kuniharibia, kamati haijaniita kuniuliza lolote bali wameamua kuchukua maamuzi wanayayofahamu wenyewe…kweli kwa sasa nalichukia soka la Bongo kwa hakika,” alisema Shija.
Shija alisema iwapo atapata barua ya adhabu yake, hatarajii kukata rufaa wala kuomba samahani kutokana na tuhuma zote, ni za kupandikizwa.
Alisema kamati ya hiyo ya ligi, inaonekana imetoa maamuzi ya ‘kitoto’ kutokana na madai yote ya kutuhumiwa kufanya ushirikina michezoni kutokuwa ya kweli.
“Nimepigiwa simu na baadhi ya viongozi wa Kanembwa JKT na kushangazwa na adhabu niliyopewa ya kufanya ushirikina dhidi yao, na hao Morani sijui niliwaroga nini,” alisema Shija.
Aidha, alisema kutokana na tuhuma alizopandikiziwa, kamati ya ligi ingemuita ili aweze kujitetea kuliko kutoa adhabu ya upande mmoja, hali ambayo inaweza kusababisha mtu asiye na hatia ‘kufungwa’.
Alisema kutokaa na mafanikio anayoyapata katika kila timu anayofundisha, wapo watu ambao hawamtakii mema na kuamua kumpandikizia chuki ili aonekane hafai.
Hata hivyo, Shija alisema kwa sasa anakumbuka wosia aliopewa na makocha marehemu Syllersaid Mziray "Super Coach" na Shaban Marijani, kuhusu ‘mizengwe’ kwa makocha soka wanaopata mafanikio nchini.