KAMATI ya Ligi ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imempiga faini ya sh. 400,000 na
kumfungia mechi sita Kocha wa Rhino Rangers, Renatus Shija kwa kushiriki
vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina na kumdhihaki mwamuzi kwenye mechi
za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Adhabu hizo zimetolewa
kwa mujibu wa kifungu cha 31(1)(a) na (b) cha Kanuni za FDL ambapo Kocha huyo
aliyeipandisha daraja Rhino Rangers kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) alifanya
vitendo hivyo kwenye mechi mbili tofauti.
Mechi hizo ni kati ya
Kanembwa JKT na Rhino Rangers iliyochezwa Februari 23 mwaka huu Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, na ile kati ya Rhino
Rangers na Morani iliyochezwa Machi 17 mwaka huu Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi
mjini Tabora.
Pia klabu ya Rhino
Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na Polisi Wanajeshi- MP kuwapiga
walinzi milangoni kwenye mechi hiyo dhidi ya Kanembwa JKT ili kupisha washabiki
wa timu hiyo waingie bure uwanjani.
Mchezaji wa timu ya Pamba
ya Mwanza, Leonard Nahole amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi nne
baada ya kumrushia chupa ya maji mwamuzi kwa madai amependelea kwenye mechi
dhidi ya Polisi Tabora iliyochezwa Machi 16 mwaka huu.
Nao wachezaji Joseph
Mapalala, Yohana Mirobo, Noel Makunja, Mkome Pastory na Rudenzi Kilinga wa
Polisi Mara wamepigwa faini ya sh. 200,000 kila mmoja na kufungiwa mechi tatu
kwa kufanya vitendo vinavyoshiria ushirikina na kumkimbiza mwamuzi kwenye mechi
dhidi ya Morani iliyochezwa Machi 9 mwaka huu. Adhabu za wachezaji hao ni kwa
mujibu wa kifungu cha 27(1)(g) cha Kanuni za FDL.
Klabu ya Villa Squad
imepigwa faini ya sh. 150,000 kwa kuchelewa uwanjani kwenye mechi yake dhidi ya
Ashanti United wakati
Majimaji imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kufanya
vurugu kwenye mechi dhidi ya Mbeya
City iliyochezwa Uwanja
wa Majimaji.
Vilevile Msimamizi wa
Uwanja wa Majimaji aliyetambulika kwa jina moja la Mapunda aliwatukana waamuzi
kwenye mechi hiyo, na suala lake
litafikishwa kwenye
Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
Pia uongozi wa Uwanja wa
Mafinga unaotumiwa na timu ya daraja la kwanza ya Kurugenzi umetakiwa kuufanyia
marekebisho, vinginevyo hautatumika kwa mechi za FDL msimu ujao.
MKUTANO WA WAANDISHI
WA HABARI
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) kesho (Aprili 11 mwaka huu) litakuwa na Mkutano na
Waandishi wa Habari. Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF.
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)