http://www.mkcomputertweaks.com/mkgroup/fkbmksb.gifMatangazo

Tangaza nasi: mkatedaniel@gmail.com, +255 7666-00 69 70, +255 655-00 69 71, +255 787- 249594

Usilikose kila Jumapili

Ijumaa, 19 Aprili 2013

TAARIFA TOKA OFISI YA TAIFA YA UKAGUZI






JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA TAIFA YA UKAGUZI
 


TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI

Ufafanuzi wa Taarifa Kuhusu Hali ya Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) zilizotolewa kwenye baadhi ya vyombo vya Habari siku ya Ijumaa tarehe 12 Aprili 2013 kutokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyotolewa Bungeni.

1.   UTANGULIZI
Siku ya Ijumaa ya tarehe 12 Aprili 2013 baadhi ya vyombo vya Habari viliandika juu ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliyoitoa Bungeni tarehe 11 Aprili, 2013 isivyo sahihi zinazohusu Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) kama ifuatavyo:
v  Kuwa Mfuko umepata hasara ya Shilingi trilioni 6.487 na hali yake kifedha ni mbaya.

v  Mfuko umekuwa ukitoa mikopo bila ya kutoza riba.

2.   UFAFANUZI
v  Kuwa Mfuko umepata hasara ya Shilingi trilioni 6.487 na hali yake kifedha ni mbaya.

Ninapenda kufafanua kuwa taarifa yangu ilivyotafsiriwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Mfuko umepata hasara ya shilingi trilioni  6.487 siyo sahihi.


Taarifa sahihi ni kuwa kiasi hicho ni nakisi (acturial deficit) ambayo imetokana na fedha ambazo ni malimbikizo ya mafao (accrued liabilities) ya Watumishi wa Umma kabla ya mwezi Julai mwaka 1999. Nakisi ya malimbikizo hayo yanatokana na tathimini iliyofanywa na mthamini (acturial valuer) M/s Genesis Actuarial Solutions kampuni kutoka Afrika Kusini.
Ninapenda kutoa ufafanuzi kuwa taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari kuwa kiasi kilichotajwa ni nakisi ya malimbikizo ya mafao ya watumishi na sio hasara ya upotevu wa fedha.

Hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2010/2011 Serikali ilikubali kuanza kurejesha mafao yaliyolipwa awali kwa wafanyakazi waliostaafu kazi kuanzia mwaka 2004.

v  Mfuko umekuwa ukitoa mikopo bila ya kutoza riba.
Kuhusiana na taarifa kuwa PSPF imekuwa ikitoa mikopo bila ya kutoza riba siyo sahihi.

Taarifa sahihi ni kwamba kiasi cha fedha kilichoonyeshwa kwenye ripoti ni mikopo (principal amount)  ambayo haikujumuisha riba na siyo kwamba mikopo hiyo haitozwi riba. Mikopo hiyo hutozwa riba na adhabu hutolewa pindi inapocheleweshwa kurejeshwa na wakopaji.

Ni imani yangu kuwa, waandishi wa habari wataendelea kuuhabarisha Umma wa Tanzania juu ya ripoti zangu kwa usahihi na pale patakapokuwa hapaeleweki, naomba mje ofisini kwangu kwa ufafanuzi.



Francis Mwakapalila
K.n.y MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI